:
Tafsiri ya Suratul-Fatiha.
Tafsiri ya Suratul-Fatiha.
Nayo iliteremka Makka
: 1 - 7 #
{بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ (1) الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ (2) الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ (3) مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ (4) إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ (5) اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ (6) صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ (7)}.
1. Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu. 2. Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu. 3. Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu. 4. Mmiliki wa Siku ya Malipo. 5. Wewe tu tunakuabudu, na wewe tu tunakuomba msaada. 6. Tuongoze katika njia iliyonyooka. 7. Njia ya wale uliowaneemesha. Siyo ya wale waliokasirikiwa, wala waliopotea.
#
{1} أي: أبتدئ بكل اسم لله تعالى؛ لأن لفظ «اسم» مفرد مضاف، فيعم جميع الأسماء الحسنى. {الله}: هو المألوه المعبود المستحق لإفراده بالعبادة، لما اتصف به من صفات الألوهية وهي: صفات الكمال. {الرحمن الرحيم}: اسمان دالان على أنه تعالى ذو الرحمة الواسعة العظيمة التي وسعت كل شيء، وعمت كل حي، وكتبها للمتقين المتبعين لأنبيائه ورسله؛ فهؤلاء لهم الرحمة المطلقة، ومن عداهم فله نصيب منها. واعلم: أن من القواعد المتفق عليها بين سلف الأمة، وأئمتها، الإيمان بأسماء الله وصفاته وأحكام الصفات، فيؤمنون مثلاً بأنه رحمن رحيم ذو الرحمة التي اتصف بها المتعلقة بالمرحوم، فالنعم كلها أثر من آثار رحمته، وهكذا في سائر الأسماء. يقال في العليم: إنه عليم ذو علم يعلم به كل شيء، قدير ذو قدرة يقدر على كل شيء.
(1) Yaani, ninaanza kwa kila Jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu; kwa sababu neno: “Jina” liko katika hali ya umoja, na limeunganishwa (na neno Mwenyezi Mungu). Kwa hivyo (huko kuunganisha) kunajumuisha majina mazuri yote. "Allah (Mwenyezi Mungu)" ni yule anayefanyiwa uungu, anayestahiki kuabudiwa yeye peke yake, kwa sababu anasifika kwa sifa za uungu, ambazo ni sifa kamilifu. "Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu" ni majina mawili yanayoonyesha kuwa yeye Mtukufu ni mwenye rehema kuu kunjufu, ambazo zimeenea kila kitu, na zinazojumuisha kila kilicho hai. Na (Mwenyezi Mungu) aliwaandikia rehema zake wachamungu wanaowafuata Manabii wake na Mitume wake. Basi, hao wana rehema kabisa. Nao wasiokuwa wao wana fungu tu kwazo (yani katika rehema hizo). Na jua ya kwamba katika misingi waliyokubaliana juu yake wale watangulizi wema wa umma huu na maimamu wake ni kuamini katika majina ya Mwenyezi Mungu na Sifa zake, na hukumu za Sifa hizo. Kwa hivyo, wanaamini kwa mfano, kwamba yeye ni Rahman (Mwingi wa Rehema), Rahim (Mwenye Kurehemu), mwenye rehema ambazo anasifika kwazo, zinazofungamana na wanaorehemewa. Kwa hivyo, neema zote ni athari katika athari za rehema yake, na vivyo hivyo katika majina mengineyo yote. Inasemwa kuhusu (jina lake) Al-‘Aliim (Mwenye elimu) kuwa yeye ni Mjuzi, Mwenye elimu, anayejua kwayo kila kitu. Qadiir (Muweza) mwenye uwezo, anayeweza kila kitu.
#
{2} {الحمد لله} هو: الثناء على الله بصفات الكمال، وبأفعاله الدائرة بين الفضل والعدل، فله الحمد الكامل بجميع الوجوه. {رب العالمين} الربُّ: هو المربي جميع العالمين، وهم من سوى الله بخلقه لهم، وإعداده لهم الآلات، وإنعامه عليهم بالنعم العظيمة، التي لو فقدوها لم يمكن لهم البقاء، فما بهم من نعمة فمنه تعالى. وتربيته تعالى لخلقه نوعان: عامة وخاصة: فالعامة هي: خلقه للمخلوقين ورزقهم وهدايتهم لما فيه مصالحهم التي فيها بقاؤهم في الدنيا، والخاصة: تربيته لأوليائه، فيربيهم بالإيمان، ويوفقهم له، ويكملهم ، ويدفع عنهم الصوارف والعوائق الحائلة بينهم وبينه. وحقيقتها: تربية التوفيق لكل خير والعصمة من كل شر، ولعل هذا المعنى هو السرُّ في كون أكثر أدعية الأنبياء بلفظ الربِّ، فإن مطالبهم كلها داخلة تحت ربوبيته الخاصة؛ فدل قوله: {رب العالمين} على انفراده بالخلق، والتدبير، والنعم، وكمال غناه، وتمام فقر العالمين إليه بكل وجه واعتبار.
(2) "Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu." Ni kumsifu Mwenyezi Mungu kwa sifa za ukamilifu, na kwa vitendo vyake vinavyozunguka kati ya kupeana fadhila na kufanya uadilifu. Kwa hivyo, ni zake sifa zote za ukamilifu kwa namna zote. "Mola Mlezi wa viumbe wa walimwengu." Mola Mlezi ni yule anayewalea walimwengu wote - nao ni kila kisichokuwa Mwenyezi Mungu - kwa kuwaumba, kuwaandalia ala, kuwaneemesha kwa neema kubwa ambazo lau kuwa watazipoteza, basi hawataendelea kuishi. Kwa hivyo, neema yoyote waliyo nayo ni kutoka kwake (Mwenyezi Mungu) Mtukufu. Na ulezi wake (Mwenyezi Mungu) Mtukufu kwa viumbe wake ni wa aina mbili: Wa kiujumla na mahususi. Ama wa kiujumla ni kuumba kwake viumbe, kuwapa riziki, na kuwaongoza katika yale yaliyo na masilahi yao ambayo ndani yake kuna kuendelea kwao kuishi katika dunia. Nao (ulezi wake) mahususi ni kulea kwake vipenzi wake; kwa kuwalea kwa imani, na kuwawezesha kuifikia (imani), na kuwakamilishia imani, na kuwaepushia yale yanayoweza kuwatoa katika imani, na vizuizi vinavyozuia kati yao na Yeye. Na uhakika wake ni kuwalea kwa kuwawezesha kufikia kila la heri, na kuwahifadhi kutokana na kila shari. Na huenda hii maana ndiyo siri iliyofanya dua nyingi za manabii kuwa na neno "Mola Mlezi." Kwa maana, mahitaji yao yote yanaingia ndani ya ulezi wake mahususi. Kwa hivyo, kauli yake "Mola Mlezi wa walimwengu" ikaashiria upweke wake katika kuumba, kuendesha mambo, kuneemesha, na kujitosheleza kwake kikamilifu, na kumhitaji kwa viumbe kabisa na kwa namna zote na kuzingatia kwote.
#
{4} {مالك يوم الدين} المالك: هو من اتصف بصفة الملك التي من آثارها أنه يأمر وينهى، ويثيب ويعاقب، ويتصرف بمماليكه بجميع أنواع التصرفات وأضاف الملك ليوم الدين، وهو يوم القيامة، يوم يدان الناس فيه بأعمالهم خيرها وشرها؛ لأن في ذلك اليوم يظهر للخلق تمام الظهور، كمال ملكه وعدله وحكمته وانقطاع أملاك الخلائق، حتى أنه يستوي في ذلك اليوم الملوك والرعايا والعبيد والأحرار، كلهم مذعنون لعظمته خاضعون لعزته منتظرون لمجازاته راجون ثوابه خائفون من عقابه، فلذلك خصه بالذكر، وإلا فهو المالك ليوم الدين وغيره من الأيام.
(4) "Mmiliki wa Siku ya Malipo." Al-Malik ni yule anayesifika na sifa ya kumiliki, ambayo miongoni mwa athari zake ni kuwa anaamrisha na kukataza, na analipa mazuri na anaadhibu, na anawaendesha wale anaowamiliki kwa kila aina ya kuendesha. Na amefungamanisha umiliki na Siku ya Malipo, nayo ni Siku ya Qiyama, siku ambayo watu watahukumiwa ndani yake kwa matendo yao, mema yake na mabaya yake. Kwa sababu, siku hiyo, viumbe watadhihirikiwa katika sura kamili, ukamilifu wa umiliki wake, uadilifu wake, hekima yake, na kukatika kwa miliki za viumbe kwa kiasi kwamba siku hiyo; wafalme, raia, watumwa, na watu huru watakuwa sawa. Wote watatii kwa sababu ya ukuu wake, na watanyenyekea sababu ya Nguvu zake, wakingoja malipo yake, wakitaraji malipo yake mazuri, na wakihofu adhabu yake. Na kwa sababu hiyo, aliitaja hususan. Vinginevyo, yeye ndiye mmiliki wa Siku ya Malipo na siku nyinginezo.
#
{5} وقوله: {إياك نعبد وإياك نستعين}؛ أي: نخصك وحدك بالعبادة والاستعانة، لأن تقديم المعمول يفيد الحصر وهو إثبات الحكم للمذكور ونفيه عمّا عداه؛ فكأنه يقول: نعبدك، ولا نعبد غيرك، ونستعين بك، ولا نستعين بغيرك، وتقديم العبادة على الاستعانة من باب تقديم العام على الخاص، واهتماماً بتقديم حقه تعالى على حق عبده. والعبادة: اسم جامع لِمَا يحبه الله ويرضاه من الأعمال والأقوال الظاهرة والباطنة، والاستعانة هي: الاعتماد على الله تعالى في جلب المنافع ودفع المضار، مع الثقة به في تحصيل ذلك. والقيام بعبادة الله والاستعانة به هو الوسيلة للسعادة الأبدية والنجاة من جميع الشرور، فلا سبيل إلى النجاة إلا بالقيام بهما، وإنما تكون العبادة عبادةً إذا كانت مأخوذة عن رسول الله - صلى الله عليه وسلم - مقصوداً بها وجه الله، فبهذين الأمرين تكون عبادة، وذكر الاستعانة بعد العبادة مع دخولها فيها؛ لاحتياج العبد في جميع عباداته إلى الاستعانة بالله تعالى؛ فإنه إن لم يعنه الله لم يحصل له ما يريده من فعل الأوامر واجتناب النواهي.
(5) Na kauli yake, "Wewe tu tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada." Yaani, tunakufanyia wewe peke yako ibada zetu, na kukuomba msaada. Kwa sababu, kutanguliza mwathiriwa (yaani, “Wewe tu”) kunamaanisha kuthibitisha kitu, nako ni kuthibitisha hukumu kwa aliyetajwa, na kumkanusha kwa mwingine asiyekuwa yeye. Ni kana kwamba anasema: “Tunakuabudu wewe, na wala hatumuabudu asiyekuwa Wewe. Na tunakuomba msaada, na wala hatumwombi msaada asiyekuwa Wewe.” Na kutanguliza kutaja ibada kabla ya kuomba msaada ni katika mlango wa kutanguliza yaliyo ya jumla kabla ya yale mahususi, na kwa sababu ya kuzingatia kutanguliza haki yake (Mwenyezi Mungu) Mtukufu mbele ya haki ya mja wake. Na ibada ni neno linalojumuisha kila akipendacho Mwenyezi Mungu na anakiridhia katika vitendo na maneno, ya dhahiri na ya siri. Na kutaka msaada ni kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kuleta manufaa, na kuyazuia yenye kudhuru pamoja na kumuamini Yeye katika kuyatafuta hayo. Na kumwabudu Mwenyezi Mungu na kumwomba msaada ndiyo njia ya kufikia kufaulu kwa milele, na kuokoka kutokana na shari zote. Kwa hivyo, hakuna njia yoyote ya kuokoka isipokuwa kwa kuyafanya yote mawili. Na kwa hakika, ibada huwa ibada tu ikiwa itachukuliwa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani ziwe juu yake, na kwa kukusudia kwayo kumridhisha Mwenyezi Mungu. Na kwa haya mambo mawili ndiyo ibada huwa. Na alitaja kuomba msaada baada ya ibada ijapokuwa kuomba msaada kunaingia humo (katika ibada); kwa sababu mja katika ibada zake zote anahitaji kuomba msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwani, Mwenyezi Mungu asipomsaidia, hatapata anachotaka miongoni mwa kufanya maamrisho na kuacha makatazo.
Kisha (Mwenyezi Mungu) Mtukufu akasema:
#
{6} {اهدنا الصراط المستقيم}؛ أي: دلنا وأرشدنا، ووفقنا إلى الصراط المستقيم، وهو الطريق الواضح الموصل إلى الله وإلى جنته، وهو معرفة الحق والعمل به، فاهدنا إلى الصراط، واهدنا في الصراط، فالهداية إلى الصراط لزوم دين الإسلام وترك ما سواه من الأديان، والهداية في الصراط تشمل الهداية لجميع التفاصيل الدينية علماً وعملاً؛ فهذا الدعاء من أجمع الأدعية وأنفعها للعبد؛ ولهذا وجب على الإنسان أن يدعو الله به في كل ركعة من صلاته لضرورته إلى ذلك؛ وهذا الصراط المستقيم هو:
{6} "Tuongoe katika njia iliyonyooka." Yaani tuonyeshe, tuongoze, na utuwezeshe kuifikia njia iliyonyooka. Nayo ni njia iliyo wazi inayofikisha kwa Mwenyezi Mungu na kwa Pepo yake. Nayo ni kujua haki na kuifanyia kazi. Basi tuongoze kuelekea kwenye hiyo njia, na utuongoze katika hiyo njia. Na kuongoza kuelekea kwenye hiyo njia ni kushikamana na dini ya Uislamu na kuacha zisizokuwa hiyo miongoni mwa dini. Nako kuongoza katika njia hiyo kunajumuisha kuongoka katika maelezo yote ya undani ya kidini, kwa elimu na vitendo. Na dua hii ni mojawapo ya dua zenye kujumuisha mno, na yenye kumnufaisha mja zaidi. Na ndiyo maana ni lazima kwa mtu amwombe Mwenyezi Mungu kwayo katika kila rakaa ya swala yake, kwa sababu yeye analihitaji hilo zaidi. Na njia hii iliyonyooka ndiyo:
#
{7} {صراط الذين أنعمت عليهم} من النبيين والصديقين والشهداء والصالحين {غير} صراط {المغضوب عليهم} الذي عرفوا الحق وتركوه كاليهود ونحوهم، وغير صراط {الضالين} الذين تركوا الحق على جهل وضلال كالنصارى ونحوهم.
{7} “Njia ya wale uliowaneemesha” miongoni mwa Manabii, na Masiddiqi (watu wakweli), na Mashahidi, na Watu wema. “Siyo” njia ya “wale waliokasirikiwa,” wale waliojua haki na wakaiacha kama vile Mayahudi na mfano wao. Na siyo njia ya wale “waliopotea” ambao waliacha haki kwa ujinga na upotovu kama vile Wakristo na mfano wao.
Licha ya ufupi wake, sura hii imekusanya yale ambayo sura yoyote katika sura za Qur-ani haijakusanya. Imekusanya aina tatu za Tawhidi: Tawhidur-Rububiyya (kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika uungu wake) inachukuliwa kutoka kwa kauli yake “Mola Mlezi wa walimwengu.” Na Tauhidul-Uluhiyya, ambayo ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu katika ibada inachukuliwa kutoka kwa neno “Allah (Mwenyezi Mungu),” na kutoka kwa kauli yake “Wewe tu tunakuabudu.” Na Tawhidul-Asmaa was-Swifaat, ambayo ni kuthibitisha sifa za ukamilifu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambazo alijithibitishia yeye Mwenyewe, na alizomthibitishia Mtume wake, bila Ta'atwil (kuzikanusha), wala Tamthil (kuzipigia mfano), wala Tashbih (kufananisha). Na neno “sifa njema zote” ndilo limeashiria hilo kama ilivyotangulia. Na (sura hii pia) inajumuisha uthibitisho wa unabii katika kauli yake, “Tuongoe njia iliyonyooka”, kwa sababu hilo haliwezekani bila ya kutuma ujumbe. Na ina uthibitisho wa malipo kwa matendo katika kauli yake “Mmiliki wa Siku ya Malipo”, na kwamba malipo yatakuwa kwa uadilifu, kwa sababu neno “diin” linamaanisha kulipa kwa uadilifu. Na inajumuisha uthibitisho wa Qadar (makadirio ya Mwenyezi Mungu), na kwamba mja ndiye mtendaji halisi, tofauti na Al-Qadariyya (wanaopinga kuwa mwanadamu anatenda kihalisi) na Al-Jabriyya (wanaosema kuwa mwanadamu hatendi chochote, lakini Mwenyezi Mungu ndiye humlazimisha kutenda). Bali inajumuisha jibu kwa watu wote wa bid’a (wanaozua katika dini) na upotovu katika kauli yake “Tuongoe njia iliyonyooka;” kwa sababu ni kujua haki na kuifanyia kazi. Na kila mwenye kuzua na kupotea, basi yeye yuko kinyume na hilo. Na inajumuisha kumpwekeshea Mwenyezi Mungu Mtukufu dini katika kumuabudu na kumuomba usaidizi, katika kauli yake; “Wewe tu tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada.” Basi sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.